Shalom, Jina la Mungu mwokozi Wetu libarikiwe, ni wakati mwingine tena ambao Mungu ametupa kibari cha kujifunza maneno yake ya uzima, karibu!
JINA LAKO LIMEANDIKWA KATIKA KITABU CHA UZIMA?
Swali hili huwenda likawa geni kwako, yaani ndiyo mara yako ya kwanza kulisikia, au pengine haufahamu kuhusu kitabu hiki cha uzima kinachozungumzia hapo. Lakini yote katika yote, ukiwa unafahamu au hufahamu, basi ni vyema tukakumbushana na kufundishana ili sote kwa pamoja tupate kuifikia ahadi ya maisha ya umilele, hiyo ni kulingana na maagizo ya Mungu Wetu kama neno lake lisemavyo kuwa “Neno lake likae kwa wingi ndani yetu katika hekima yote tukifundishana na kuonyana”
Kitabu cha uzima kinachozungumziwa sio kitabu ambacho kinapumua na kuvuta pumzi kama mwanadamu (kinahema), hapana, bali kitabu cha uzima ambcho jina lako linapaswa kuwepo ni hiki
Tusome
Ufunuo 3:5 Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika KITABU CHA UZIMA, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake.
Kitabu cha uzima ni kitabu kilichobeba maisha ya mwanadamu aliyeweza kuishi maisha matakatifu yanayoendana na maneno ya Mungu yaani maandiko matakatifu, kitabu hicho kazi yake kuu ni kulinganisha matendo ya mwanadamu na maandiko matakatifu kama yanakwenda sawa sawa na maandiko. Mfano mzuri ni pale mtu anapotaka kununua bidhaa labda mchele, yule muuzaji hawezi tu kumpa bidhaa yake kisa ametaja kiasi anachotaka, lazima atapima kwanza ndipo ampe, na kifaa kitakacho tumika kupimia huwa ni mizani kwa sababu kifaa hiki husaidia kulinganisha usawa wa bidhaa na kilo, na kabla ajampatia mteja wake mchele lazima atauweka katika mizani kisha ataweka mawe ya kilo, hili aweze kulinganisha je! mchele na mawe ya kilo yanaendana? na ikionekana kuwa ni sawa basi mteja hupewa bidhaa yake.
Vivyo hivyo na maisha yetu kwa Mungu Wetu, Yeye huyapima katika neno lake akitazama je maisha tunayoishi yapo sawa na maagizo Yake? Kama yakionekana kuwa ni sawa basi moja kwa moja Jina la mtu huyo linaandikwa katika kitabu cha uzima na ikiwa anaenenda tofauti na neno basi Jina la mtu huyo haliwezi onekana katika kitabu cha uzima
Ufunuo 21:27 Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali WALE WALIOANDIKWA KATIKA KITABU CHA UZIMA CHA MWANA-KONDOO.
Mwanadamu fahamu hili, maisha yako ni kitabu na matendo yako ni kalamu inayoandika kumbukumbu ya maisha yako ya hapa duniani kama yanaendana na maneno ya Mungu, maandiko yanatueleza katika kitabu kile wataandikwa wale tu walio mwamini Kristo na kushinda tamaa za ulimwengu na siyo wanyonge, walioshindwa kuishi maisha matakatifu
Je! maisha yako unayaandika namna gani kwa kadri Mungu anavyokupa pumzi kila siku, kumbuka waonyonge wanaozungumziwa hapo si watu ambao hawajala chakula kwa mda mrefu au watu wenye magonjwa, hapana bali wanyonge wanaozungumziwa hapo ni watu walioshindwa kuishi maisha matakatifu, na matendo yao siku zote yalionekana kuwa madhaifu kwa kutenda machukizo na mambo ya ulimwengu huu, na mfano wa mambo hayo ni haya
Wagalatia 5:19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,
20 ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi
21 husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.
Ikiwa bado upo katika makundi haya tambua kabisa jina lako bado halipo katika kitabu cha uzima, Neno la Mungu linasema “yeye ashindae ndiye atakaye andikwa katika kitabu cha uzima” mtu
aliyeshinda tamaa za duniani hii na kuweza kuliishi neno mtu huyu jina lake ndiyo lipo kitabuni.
Pia unaposema umeokoka lakini matendo yako yanakuelekeza na kukushuhudia kuwa unaenda motoni, unapata faida gani kusema umeokoka? maana mtu anaposema nimeokoka anamaanisha kuwa amekataa maisha ya dhambi na anahitaji kuifikia ahadi ile ya Mungu ya mbingu mpya na nchi mpya, lakini kama upo katika wokovu na maisha yako ni yale yale ya kidunia yaani uzinzi wewe, uongo wewe, wivu wewe, fitina na chuki ni wewe, n.k, ukiwa na mambo kama haya katika wokovu wako Jina lako utalikuta katika kitabu kingine kinachoitwa “kitabu cha hukumu” hivyo yakupasa ujipambambanue sana maana ule mwisho wa maisha yako ukifika utakuwa mgeni wa nani kwa kuichezea neema ya Mungu kwa kujiwekea maisha ya sinema katika wokovu? jifikirie utakuwa wapi?.
Tambua kuwa neema hii ya wokovu haitadumu milele bali kuna wakati haitakuwepo, sasa ni wakati wa kuchunguza sana maisha yako ya wokovu na utazame wapi umerudi nyuma kisha utengeneza tena uhusiano wako na Mungu kwa kuishi sawa sawa na Neno lake vinginevyo JEHANAMU itakuwa juu yako
Na kwa wewe ambaye bado ujampokea Kristo vivyo hivyo nawe usikawie neema haidumu, hakikisha Jina lako linapatikana katika kitabu cha uzima kwa kukubali kumpokea Yesu na kumfanya kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako,
Warumi 10:9 Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.
10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.
Hakiki maisha yako leo na ujitazame mwenyewe endapo ukifa au Kristo akirudi leo utakuwa wapi? Jibu unalo.
JITAHIDI MAISHA YAKO YAENDANE NA NENO LA MUNGU
Maran atha
Mada zinginezo:
Je! Ni wanawake gani wanazungumziwa katika (Zaburi 68:11)?
Mtupe chini Yezebeli kama unataka kuwa upande wa Mungu
MAANA YA KUOTA UPO MAKABURINI.