Makaburi ni mahali ambapo wanalazwa watu waliokufa… Hivyo kuota upo makaburini sio ishara nzuri. Katika biblia kuna wakati Bwana alikutana na mtu mmoja anayeishi makaburini, ambapo makazi yake yalikuwa ni kule siku zote, haondoki..maandiko yanatuambia mtu yule alikuwa ameingiliwa na pepo wengi sana..na lengo ni kuangamiza na kuua.
Utauliza nimejuaje hilo, ukisoma habari ile utaona yale mapepo baada ya kumtoka yule mtu yaliwaingia wale nguruwe na kuwapeleka baharini..
Marko 5 :1-15
“1 Wakafika ng’ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi.
2 Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu;
3 makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu ye yote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo;
4 kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunja-vunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda.
5 Na sikuzote, usiku na mchana, alikuwako makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikata-kata kwa mawe.
6 Na alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia;
7 akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese.
8 Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu.
9 Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tu wengi.
10 Akamsihi sana asiwapeleke nje ya nchi ile.
11 Na hapo milimani palikuwa na kundi kubwa la nguruwe, wakilisha.
12 Pepo wote wakamsihi, wakisema, Tupeleke katika nguruwe, tupate kuwaingia wao.
13 Akawapa ruhusa. Wale pepo wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi lote likatelemka kwa kasi gengeni, wakaingia baharini, wapata elfu mbili; wakafa baharini.
14 Wachungaji wao wakakimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani. Watu wakatoka walione lililotokea.
15 Wakamwendea Yesu, wakamwona yule mwenye pepo, ameketi, amevaa nguo, ana akili zake, naye ndiye aliyekuwa na lile jeshi; wakaogopa”.
Umeona?. Hivyo ukiota upo makaburini ni ishara kuwa hali yako ya kiroho sio nzuri..Lakini habari njema ni kwamba Yupo Yesu anayetengeneza mambo, na kuyarudisha katika mstari.
Siwezi kujua kwa undani maisha yako ya kiroho, pengine upo dhambini, umefungwa na mapepo, umefungwa na roho za ulevi, uzinzi, uuaji, wizi, tamaa mbaya n.k. Zote hizo ni roho za makaburini..mahali pa wafu!..kiroho wewe umekufa, lakini Bwana Yesu anaweza kukurejeshea uhai wako na ukawa mzima kiroho, na ukatoka huko makaburini kama alivyomtoa yule mtu aliyekuwa na pepo wale.
Yeye mwenyewe alisema..
Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu”;
Unachopaswa kufanya sasa ikiwa unataka kumkaribisha Yesu maishani, ni kujitenga mwenyewe kisha kutubu dhambi zako kwa Bwana Yesu, unatubu kwa kumaanisha kuziacha kabisa, kisha baada ya hapo Bwana atakusamehe na kuingia maishani mwako, na hatua inayofuata ni wewe kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Bwana Yesu, na Roho Mtakatifu atakuongoza katika kweli ya maandiko.