Unapoota umechelewa kwenye harusi, hiyo ni ndoto ya tahadhari kutoka kwa Bwana.
Ni nadra sana zote za namna hii kuwa na tafsiri ya ndoa halisi za kimwili, nyingi zinafunua ndoa za kiroho.
Kibiblia sisi watu wa Mungu tunafananishwa na wanawali na Kristo ni Bwana arusi, na karamu yetu (yaani harusi) itafanyika mbinguni.
Hivyo kama umeota umechelewa kwenye harusi aidha yako mwenyewe au ya mwingine, tafsiri yake ni kwamba UMEJIWEKA MBALI NA KRISTO AU UMERUDI NYUMA KIROHO PAKUBWA SANA.
Hivyo unyakuo wa kanisa utakapopita kama utakuwa hujajisogeza karibu na Kristo kwa viwango anavyotaka yeye utaachwa hutakwenda mbinguni kwenye Harusi yake/karamu yake.
Hebu tusome habari ifuatayo kwenye biblia…
Mathayo 25:1-13
[1]Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi.
[2]Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye busara.
[3]Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao;
[4]bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao.
[5]Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi.
[6]Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki.
[7]Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao.
[8]Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika.
[9]Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie.
[10]Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa.
[11]Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie.
[12]Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi.
[13]Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa.
Umeona?.. Hapo hao wanawali wapumbavu walivyoikosa karamu?
Vivyo hivyo Mungu anakuonesha kuwa utaikosa karamu ya mbinguni ukiendelea kuwa vuguvugu. Hivyo chunguza maisha yako ni wapi umezembea, au ni wapi umerudi nyuma kiimani. Na kama hujampokea Yesu kabisa ni dhahiri kuwa hutaingia karamuni siku ile.
Je maisha yako ni ya ulevi?, Uasherati, wizi, utukanaji, usengenyaji, uvaaji mbaya kama vimini, wigi, na suruali kwa mwanamke n.k. Jua hayo ndio baadhi ya mambo yatakayomfanya mtu achelewe karamuni.
Maran atha.
0789001312/ 0693 036 618