FUNDISHO MAALUMU KWA WAZAZI NA WALEZI
Umeshawahi kujiuliza ni kwanini dhambi ya uzinzi na uasherati ndio iliyo na kasi kubwa sana sasa hivi juu ya uso wa nchi? Si kwa watoto wadogo, si kwa vijana, si kwa wazee, wote ni watamanifu, si kwa maskini si kwa matajiri, si kwa viongozi, wote ni watu wa kutamani, ulishawahi jiuliza ni Kwa sababu gani? Jibu ni kwamba, kwa sehemu kubwa hayo yote yanachangiwa sana na wazazi na walezi KWA KUWANAJISI MABINTI ZAO bila kufahamu, ndio! Jambo hili Iinaweza likakushangaza na kukusitusha kidogo lakini ukweli ndivyo ulivyo, wazazi wetu si wakamilifu ni waovu pia (ndivyo biblia inavyosema), na ndio maana na wao wanahitaji kutubu na kubatizwa kwa jina la Yesu Kristo.
Matayo 7:11 Basi IKIWA NINYI, MLIO WAOVU, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?
Leo hii kwenye mitandao ya kijamii picha chafu na za ovyo zinazoongoza ni za mabinti walionajisiwa na wazazi na walezi wao, kwenye vipindi vya television na luninga wanaovaa nguo za uchi na nusu uchi ni mabinti, kwenye mavyuo mabinti ndio wanaoongoza kuvaa nguo za ovyo, kwenye taasisi za kazi kama mabenki na sehemu za usafirishaji mfano airports, mabinti ndio wanaovaa suruali zinazochora makalio yao na maungo yao yote, kwenye kumbi za anasa mfano makasino, bar, viwanja vya michezo, night clubs n.k, wote ni mabinti walionajisiwa na walezi wao kwa kutokufahamu.
Biblia Inasema katika
Walawi 19:29 USIMNAJISI BINTI YAKO, ILI KUMFANYA AWE KAHABA; isiwe hiyo nchi kuuandama ukahaba, NA NCHI KUJAWA NA UOVU MKUU.
Wazazi wengi na walezi wengi leo hii kwa kukuosa maarifa ya Mungu (kutokana na uvivu wa kuyatafuta na wengine kuyakataa kabisa), wanajikuta pasipo kujua wakiwanajisi mabinti zao na kuwafanya makahaba kitu ambacho kinapelekea dhambi ya uzinzi na uasherati kukua kwa kasi sana leo hii.
Sasa yafuatayo ni mambo ambayo wazazi na walezi wanayafanya na kuwanajisi mabinti zao kwa kutokujua na kusababisha ukuaji na uongezekaji mkubwa wa uzinzi na uasherati.
1. KURUHUSU BINTI YAKO KUVAA SURUALI.
Hili ni moja ya jambo ambalo wazazi wengi na walezi wengi sana hawalifahamu, kumbuka, asili ya mwili wa binti yako au mwanamke yoyote yule ni kutamanika (Mathayo 5:28), hivyo, binti yako anapovaa suruali maungo yake na shepu yake yote inakuwa wazi kwa wanaume wanaomtaza, hivyo, inapelekea binti yako kuzini na mamia ya watu mioyoni mwao kwa kumtamani maungo yake na shepe yake tu pekee, hivyo unamfanya kuwa kahaba kwa kuzini na watu hao mioyoni mwao. Wazazi na Walezi wengi kwa kushindwa kuzuia hili, imepelekea leo hii uovu kuwa mkubwa na mmomonyoka wa maadili kuongezeka kila kona kutokana na mabinti kuvaa suruali ambazo zinawatamanisha wanaowataza na kufanya idadi kubwa ya makahaba kuongezeka (kwa sababu hakuna tofauti kati ya hao mabinti na makahaba, wote wanavaa sawa tu).
Wewe kama mzazi na mlezi wa kikristo unapaswa utambue kuwa, kazi yoyote ile itakayomlazimu binti yako kuvaa suruali ni najisi, na utakapomrusuhu kwenda kuifanya utakuwa unamnajisi binti yako na kumfanya kuwa machukizo kwa Mungu.
Kumbukumbu La Torati 22:5 Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume, wala mwanamume asivae mavazi ya mwanamke; kwa maana kila afanyaye mambo hayo ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako.
2. KURUHUSU BINTI YAKO KUVAA NGUO FUPI (VIMINI)
Wewe kama mzazi au mlezi wa Kikristo, unapomruhusu binti yako kuvaa nguo fupi (vimini), tambua kuwa unamnajisi na kumfanya kahaba bila kujua. Kumbuka, kichocheo moja wapo cha uzinzi na uasherati leo hii ni uvaaji mbaya kwa mabinti sehemu mbali mbali kama vile kwenye vipindi vya television na mitaani, binti yoyote yule anapovaa nguo fupi mapaja yake yote (ambayo yalipaswa kusitiriwa), yanakuwa hadharani na kuchochea uasherati kwa wanao mtazama, na endapo huyo binti akiinama na hicho kimini ndio kabisa nguo ya ndani inaweza hata kuonekana, sasa kwa unajisiwaji huu wa mabinti unategemea vipi uzinzi na uasherati usiongezeke katika jamii? Je! kunakuwa na utofauti wowote ule kati ya hao mabinti na makahaba wanaojiuza gizani na kwenye makasino? Mzazi wa kikristo, binti yako anapaswa kuvaa Mavazi ya heshima na adabu yanayositiri mwili wake (lihakikishe hilo juu yake na kulifuatilia kila siku).
1 Timotheo 2:9 Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa MAVAZI YA KUJISITIRI, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;
3. KURUHUSU BINTI YAKO KUISHI NA MWANAUME PAMOJA NA HUKU HAWAJAFUNGA NDOA.
Kufanya tendo la ndoa kabla ya kufunga ndoa ni uasherati na ni dhambi mbele za Mungu, wazazi wengi na walezi wengi ambao ni wakristo, wanalitambua hili sana lakini cha ajabu ni kwamba, wanalifumbia jambo hili macho na kuwanajisi mabinti zao kwa kuwaruhusu kabisa kwenda kuishi na kulala na wanaume ambao hawajafunga nao ndoa (mahusiano kama haya ni dhambi mbele za Mungu na wahusika wanapaswa kutubu na kufuata kanuni za kibiblia vingine ni kuzimu endapo wakifa katika hali hiyo). Aina hii ya mahusiano ndio iliyoenea sana sasa hivi na walezi ndio chanzo. Mzazi/Mlezi, usimnajisi binti yako na kumfanya kuwa kahaba, fuata misingi ya Kikristo, hakuna kukaribiana kabla ya ndoa
Matayo 1:18 Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake ALIPOKUWA AMEPOSWA NA YUSUFU, KABLA HAWAJAKARIBIANA, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu.
4. KURUHUSU BINTI YAKO KUWEKA MAPAMBO MWILINI MWAKE.
Unapomruhusu binti yako kuweka mapambo mwilini mwake kama vile make ups, kupaka wanja machoni, lipstick midomoni n.k, tambua kuwa unamnajisi na kumfanya kuwa kama kahaba. Mwanamke yoyote anayetumia vitu hivyo hana tofauti na kahaba kwa sababu makahaba ndio wanaovitumia vitu hivyo kwa lengo la kuwavutia na kuwatamanisha wateja wao (wanaume) kwa ajili ya kazi yao ya ukahaba. Je! Na wewe binti yako ni chombo cha kuwavutia na kuwatamanisha wateja waje kufaya nae ukahaba?
Katika biblia, mwanamke aliyefanya mambo hayo ni Yezebeli, ambaye alikuwa ni mzinzi na mchawi (2 Wafame 9:22), na tena imeandikwa, mwanamke huyu alipopata habari juu ya ujio wa mtumishi wa Mungu Yehu, alienda kupaka wanja machoni mwake na kupamba nywele zake na kuchungulia dirishani kwa lengo la kumshawishi na kumtamanisha mtumishi wa Mungu Yehu kingono kwa sababu ndivyo makahaba wanavyofanya.
2 Wafalme 9:30 Hata Yehu alipofika Yezreeli, Yezebeli akapata habari; AKATIA WANJA MCHONI MWAKE, AKAPBA KICHWA CHAKE, AKACHUNGULIA DIRISHANI.
5. KURUHUSU BINTI YAKO KUJIPAMBA MWILI WAKE KWA LULU NA DHAHABU
Hii inajumuisha hereni zote za masikioni (kubwa au ndogo), vipini puani na kwenye ulimi, mikufu na cheni shingoni, mikufu miguuni (vikuku), shanga katika kiuno cha binti yako n.k. Mpendwa mzazi na mlezi, unaporuhusu vitu hivi kwa binti yako, fahamu kuwa unamnajisi na kumfanya kuwa kahaba kwa sababu katika biblia, wanawake wote wanaoukiri uchaji wa Mungu wamekatazwa kujipamba kwa hivyo.
1 Timotheo 2:9 Vivyo hivyo WANAWAKE na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; SI KWA KUSUK NYWELE, WALA KWA DHAHABU NA LULU, wala kwa nguo za thamani;
10 bali kwa matendo mema, KAMA IWAPASAVYO WANAWAKE WANAOUKIRI UCHAJI WA MUNGU.
Lakini wanawake wote wasioukiri uchaji wa Mungu na makahaba ndio wanaojipamba kwa lulu, dhahabu, n.k, kama mtume Yohana alivyooneshwa katika maono taswira ya mwanamke aliyejaa mchukizo na mama wa makahaba alivyopampwa
Ufunuo 17:4 NA MWANAMKE YULE alikuwa amevikwa nguo ya rangi ya zambarau, na nyekundu, AMEPAMBWA KWA DHAHABU, NA KITO CHA THAMANI, NA LULU, naye alikuwa na kikombe cha dhahabu mkononi mwake, kilichojawa na machukizo, na machafu ya uasherati wake.
5 Na katika kipaji cha uso wake alikuwa na jina limeandikwa, la siri, BABELI MKUU, MAMA WA MAKAHABA NA MACHUKIZO YA NCHI.
Unaona hapo? Mwanamke anayeukiri uchaji wa Mungu kakatazwa kujipamba kwa hivyo lakini mwanamke kahaba na mama wa makahaba kapambwa kwa hivyo, kunaanisha kuwa yeye hauukiri uchaji wa Mungu, hivyo na wewe utakapomruhuau binti yako vitu hivyo unamnajisi na hauukiri uchaji wa Mungu hata kama unanena kwa lugha na kutabiri.
Hivyo, kama wewe ni mzazi au mlezi, na umetambua kuwa umekosea na umemnajisi binti yako kutokana na kutokufahamu kwako na kukosa maarifa ya Mungu, basi huna budi kutubu na kujirekebisha, na kama bado hujayakabidhi maisha yako kwa Mwokozi wa ulimwengu Yesu Kristo nafasi ni sasa, tubu na kubatizwa katika JINA LA YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.
Bwana akubariki, Shalom.
Tafadhari washirikishe wazazi na walezi wengine ujumbe huu.
Mada zinginezo:
SITIRI MWILI WAKO, USIWE CHANZO CHA MWENGINE KUTAMANI
KUVAA SURUALI NI DHAMBI KWA MWANAMKE WA KIKRISTO?
Mtupe chini Yezebeli kama unataka kuwa upande wa Mungu
Je! Ni wanawake gani wanazungumziwa katika (Zaburi 68:11)?
Mafunzo mazuri sana yanafunza na yatasaidia sana kukuza mabinti zetu kiroho
Amina sana