Bwana Yesu Asifiwe, ni wakati mwingine tena ambao Mungu ametupa kibari cha kuweza kujifunza maneno yake yanayotupa kuiifikia ahadi yake ya mbingu mpya na nchi mpya, lakini kabla ya kuendelea mbele tutajifunza maana ya neno hili “unyenyekevu“ambalo litakuwa kiini cha ujumbe wetu
Unyenyekevu ni hali ya mtu kujishusha pale anapofanya jambo fulani ambalo lilipelekea kumpa sifa fulani, au pale ambapo anajizuia kujipandisha juu wakati anapopokea sifa kutoka kwa watu kwa kitu au jambo alilolitenda kwa ustadi mzuri. Jambo hilo linaitwa “unyenyekevu”
Sawa sawa na andiko la
Mithali 29:23
[23]Kiburi cha mtu kitamshusha;
Bali mwenye roho ya UNYENYEKEVU ataheshimiwa.
Basi kwa utangulizi huo ambao umebeba kiini cha ujumbe, tunaendelea na ujumbe wetu wa leo
Kuna maneno ambayo Bwana wetu Yesu Kristo aliwajibu wayahudi, pale walipo shangaa kuona amenena maneno ya hekima ambayo hawakuwahi kuyasikia kwa viongozi wao wa dini wenye elimu wakinena maneno yale yenye hekima kama ya Bwana Yesu, lakini katika hali hiyo hiyo ya kustaajabu kwao, tunaona Bwana Yesu hakujiinua bali alinena maneno haya “mafunzo yangu si yangu bali yeye aliyenipeleka”
Yohana 7:14-16
[14] Hata ikawa katikati ya sikukuu Yesu alikwea kuingia hekaluni, akafundisha.
[15] Wayahudi wakastaajabu wakisema, Amepataje huyu kujua elimu, ambaye hakusoma?
[16] Basi Yesu akawajibu, akasema, MAGUNZO YANGU SI YANGU MIMI, ILA NI YAKE YEYE ALIYENIPELEKA.
Hapa tunajifunza kuwa, japo wayahudi walishangaa jinsi Bwana Yesu alivyowapa mafundisho mazuri ambayo hawakuwahi kuyasikia kabisa, lakini kuna jambo ambalo alilizingatia, hakujiinua juu kwa kujinadi kuona yeye ni bora kuliko hao viongozi wao wa dini, lakini badala yake alinyeyekea na kumpa Mungu UTUKUFU kwa kusema “MAFUNZO YANGU SI YANGU MIMI, ILA NI YAKE YEYE ALIYENIPELEKA.”
HII INATUFUNDISHA NINI?
Hii inatufundisha kuwa, Bwana wetu Yesu Kristo ndiyo kielelezo cha maisha yetu kama maandiko yanavyosema.
Yohana 13:15
[15] Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo.
Hivyo, kama tukishindwa kumfuata yeye mienendo yake hakika itakuwa ngumu sana kuyatimiza mapenzi ya Mungu, ebu fikiria jinsi Yesu Kristo alivyo japo alikuwa na uweza wote na hakuna jambo ambalo yeye alishindwa kulitenda, lakini alijinyenyekeza, sasa wewe mwanadamu kwanini kujiinua?
Katika maandiko tunajifunza habari ya mtu mmoja ambaye alijiinua na matokeo yake aliangukia pabaya, naye ni Mfalme Nebukadreza. Mfalme huyu kwa kujiinua kwake kupitia mafanikio yake na utawala wake kulimfanya apate hasara kubwa sana katika maisha yake, japo alipewa maonyo juu ya kujiinua kwake aache lakini hakusikia badala yake akafanywa kuwa kiumbe cha ajabu na kutupwa kondeni kama mnyama
Danieli 4:29-33
[29]Baada ya miezi kumi na miwili, alikuwa akitembea ndani ya jumba la kifalme katika Babeli.
[30] Mfalme akanena, akasema, Mji huu sio Babeli mkubwa nilioujenga mimi, uwe kao langu la kifalme, kwa uwezo wa nguvu zangu, ili uwe utukufu wa enzi yangu?
[31] Hata neno lile lilipokuwa katika kinywa cha mfalme, sauti ilikuja kutoka mbinguni, ikisema, Ee mfalme Nebukadreza, maneno haya unaambiwa wewe; Ufalme huu umeondoka kwako.
[32] Nawe utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni; utalishwa majani kama ng’ombe, na nyakati saba zitapita juu yako, hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, awaye yote.
[33] Saa iyo hiyo jambo hilo likatimizwa, likampata Nebukadreza; alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani kama ng’ombe, na mwili wake ulilowa maji kwa umande wa mbinguni, hata nywele zake zikakua, zikawa kama manyoya ya tai, na kucha zake kama kucha za ndege.
Hizo ni hasara za kushindwa kuwa mnyenyekevu, katika maisha haya tunayoishi siku zote Mungu utazama neno lake juu ya mienendo yetu, pale ambapo mtu atashindwa kuliishi neno, basi ndipo hapo atakapoenda kinyume na maagizo ya Mungu
Kila jambo ulilonalo sasa ni Mungu ndiye ameliruhusu uwe nalo, iwe ni huduma nzuri, iwe ni Karama na kipawa, uwezo wa mali, biashara nzuri, majumba mazuri, na ufahari wote unaoujua wewe, yote hayo ni Mungu ndiyo ameruhusu uyapate, hivyo usijiinue hata kidogo ukawaza akilini mwako kuwa hizo ni busara zako na hekima zako, na elimu yako, hapo utakuwa unajitafutia laana badala ya baraka, wewe jifunze tu kwa MKOMBOZI WA ULIMWENGU jinsi alivyonyenyekea, wewe mwanadamu u nani hata kujiinua na kujisifu kuwa ni uweza wako? acha kabisa tabia hiyo itakufikia pabaya, ebu mtazame Mfalme Nebukadreza jinsi alivyo angukia pabaya kutoka kuwa mtu mwenye ufahari na kuwa kama mnyama, unyenyekevu ni jambo la busara sana na la heri mbele za Mungu
Mika 6:8
[8]Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na BWANA anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa UNYENYEKEVU na Mungu wako!
Mtukuze Mungu kwa ulichokipokea acha kutafuta sifa kwa watu, kwa kutaka kujulikana sana na kuwa mtu maarufu, ukitaka hayo utaishia hapa duniani, umaarufu wako utapita, jina lako litapita, cheo chako kitapita, elimu yako itapita, umaridadi wako utapita, uzuri wako utapita nk.. lakini kama unahitaji kutembea katika baraka za Mungu, fanya hivi..
Utakapo hubiri na kufundisha vizuri watu wakabarikiwa mtukuze Mungu kwa kusema, mafunzo yangu si yangu, utakapoimba vizuri mapepo yakaripuka mpe Utukufu Mungu, utakapo jenga nyumba nzuri mpe Utukufu Mungu, utakapopata cheo kikubwa kazini au sehemu yoyote mtukuze Mungu, utapokuwa na biashara nzuri mtukuze Mungu nk…
Umtukuze Mungu kwa kila jambo kwa sababu YEYE NDIYE ALIYE KUWEZESHA UTENDE HIVYO AU UPATE HIVYO, usiruhusu kiburi kiwe ndani yako, usiruhusu kujiinua kuwe ndani yako bali ruhusu UNYENYEKEVU UWE NDANI YAKO
Yohana 3:30
[30] Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua.
Bwana atusaidie katika hili
Ubarikiwe
Mada zinginezo:
Mtupe chini Yezebeli kama unataka kuwa upande wa Mungu
UNAPOOTA UNAJIFUNGUA MAANA YAKE NINI?