Shalom, ni wakati mwingine tena Bwana Yesu ametupa nafasi ya kujifunza, akituonya na kutukumbusha maana Neno lake ni taa iongozayo miguu yetu.
Ulishawahi kukaa na kujiuliza maswali haya?…Ni nani aliye kupa afya na uzima, ni nani aliyekupa kazi, ni nani aliyekupa akili timamu, ni nani aliyekupa uwezo wa kufanya biashara uliyo nayo wakati huu, ni nani aliyekupa mke au mme, na ni aliyekupa watoto, ni nani aliyekupa uwezo wa kutembea kutoka sehemu moja na kwenda nyingine? Bila shaka kama ulishawahi kujiuliza maswali hayo naamini jibu lako moja kwa moja lilikuwa kwamba ni Mungu ametenda yote hayo, na ni kweli kabisa wala ujakosea ndivyo ilivyo Mungu ndiyo anatupa yote.. na hakuna mwanadamu anayeweza kujisifu kuwa ni yeye amefanya kwa akili zake, huyo ni muongo na anajitafutia laana.
Sasa kama tunayajua hayo yote kuwa ni Mungu ndiye anafanya kwanini sasa hatumuheshimu Mungu? Yaani tumekuwa watu wa kutoa udhuru kwa sababu ya mke au mme, watoto, kazi nk.. na tumeshindwa hata kukumbuka kuwa hapa dunia kuwepo si akili zetu wala elimu na taaluma zetu zilizotufanya tuwepo duniani bali ni Mungu muumba mbingu na nchi na vyote pia, yaani tumejisahau kabisa na kudhani mioyoni mwetu sisi ndio kila kitu, tofauti kabisa na Neno linavyosema.
Kumbukumbu la Torati 8:17-19
[17]Hapo usiseme moyoni mwako, Nguvu zangu na uwezo wa mkono wangu ndio ulionipatia utajiri huo.
[18]Bali utamkumbuka BWANA, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.
[19]Lakini itakuwa, kama ukimsahau BWANA, Mungu wako, na kuiandama miungu mingine, na kuitumikia na kuiabudu, nawashuhudia leo ya kuwa mtaangamia bila shaka.
[20]Kama vile mataifa yale ambayo BWANA anawaangamiza mbele yenu, ndivyo mtakavyoangamia; kwa sababu hamkutaka kuisikiliza sauti ya BWANA, Mungu wenu.
Ndugu, usijisifu kwa chochote kile, hivyo vyote ulivyonavyo ni Mungu tu na wala usiviabudu, ni kujitafutia kuwa mbali na Mungu.
Kuna mfano mmoja Bwana Yesu aliutoa juu ya kundi hili la watoa udhuru, hebu tujifunze jambo hapa
Luka 14:15-24
[15]Basi aliposikia hayo mmojawapo wa wale walioketi chakulani pamoja naye alimwambia, Heri yule atakayekula mkate katika ufalme wa Mungu.
[16]Akamwambia, Mtu mmoja alifanya karamu kubwa akaalika watu wengi,
[17]akamtuma mtumwa wake saa ya chakula awaambie wale walioalikwa, Njoni, kwa kuwa vitu vyote vimekwisha kuwekwa tayari.
[18]Wakaanza wote KUTOA UDHURU kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, Nimenunua shamba, sharti niende nikalitazame; tafadhali unisamehe.
[19]Mwingine akasema, Nimenunua ng’ombe jozi tano, ninakwenda kuwajaribu; tafadhali unisamehe.
[20]Mwingine akasema, Nimeoa mke, na kwa sababu hiyo siwezi kuja.
[21]Yule mtumwa akaenda, akampa bwana wake habari ya mambo hayo. Basi, yule mwenye nyumba akakasirika, akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika njia kuu na vichochoro vya mji, ukawalete hapa maskini, na vilema, na vipofu, na viwete.
[22]Mtumwa akasema, Bwana, hayo uliyoagiza yamekwisha tendeka, na hata sasa ingaliko nafasi.
[23]Bwana akamwambia mtumwa, Toka nje uende barabarani na mipakani, ukawashurutishe kuingia ndani, nyumba yangu ipate kujaa.
[24]Maana nawaambia ya kwamba katika wale walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu.
Umeona hapo? Ipo hatari kubwa sana kwa watu wanasema wameokoka lakini ndiyo watu maarufu kutoa udhuru katika kazi ya Bwana na ibadani, jihakiki sana maisha yako ya wokovu kabla hatari kubwa haijaingia maishani mwako, ya kutupwa nje na Bwana hivyo
Penda ibaada, penda kukusanyika na watakatifu wenzako, hebu MHESHIMU MUNGU WAKO maana yeye ni zaidi ya hivyo vitu vyako pasipo yeye huwezi kuvifanya, pona leo juu ya hili na urudi katika mstari wa wokovu kwa viwango vingine, dhambi ya kutoa udhuru ife kwako…. ukimheshimu Mungu naye atakuheshimu, lakini ukikaidi utakuwa si kitu mbele za Mungu
1 Samweli 2:30
[30]Kwa sababu hiyo, BWANA, Mungu wa Israeli, asema, Ni kweli, nalisema ya kuwa nyumba yako, na nyumba ya baba yako itakwenda mbele zangu milele; lakini sasa BWANA asema, Jambo hili na liwe mbali nami; kwa maana wao wanaoniheshimu nitawaheshimu, na wao wanaonidharau watahesabiwa kuwa si kitu.
Bwana atusaidie katika hili.