Kabla ya kuendelea na namna ya kuishi maisha matakatifu, tuelewe kwanza nini maana ya maisha matakatifu
Maisha matakatifu ni maisha yasiyokuwa na uchafu ndani yake, maisha ambayo yanaendana kwa kuyafanya mapenzi ya Mungu kama alivyo agiza katika neno lake, pia ni maisha yasiyotawaliwa na mawazo maovu mfano uzinzi, usherati, wizi, ugomvi, fitina, uongo, chuki, hasira, nk.. bali wakati wote maisha matakatifu yanakuwa yapo sambamba na neno la Mungu pasipo maigizo wala kujionyesha bali katika utiifu na unyenyekevu mkubwa, hayo ndiyo maisha matakatifu, na kila Mkristo aliyeokoka anapaswa kuishi maisha hayo ya utakatifu na kuwa mtakatifu kama kama Mungu Mwenyewe.
1 petro 1: 16 Kwa maana imeandikwa Mtakuwa watakatifu kwa kuwa Mimi ni mtakatifu
Sasa mtu yo yote yule anapokuwa bado hajapata wokovu, kuishi maisha ya utakatifu au kuwa mtakatifu kwake ni ngumu sana kwa sababu, maisha matakatifu hayatengenezwi kiwandani wala hayauzwi dukani kusema kwamba mtu akihitaji kununua anakwenda, haipo hivyo bali kuna kanuni na taratibu zote za kuishi maisha matakatifu zinapatikana katika Neno la Mungu tu na kwa msahada wa Roho Mtakatifu (Hivyo kuna umuhimu mkubwa sana wa mtu kumkimkiri Yesu Kristo na kupokea Roho wake)
Inaaminika na watu wengi leo hii duniani na hata baadhi ya wakristo kwamba hakuna mtu anayeweza ishi maisha matakatifu katika dunia ya sasa, kitu ambacho si sawa kabisa na kipo tofauti na neno linalosema
1 petro 1: 16 Kwa maana imeandikwa Mtakuwa watakatifu kwa kuwa Mimi ni mtakatifu
Na tena ipo misemo ambayo imeibuka kwa watu wa kizazi hiki kwa kusema “ulimwengu huu wa sasa kuishi maisha mtakatifu ni jambo gumu kabisa kwa sababu mambo yamekuwa mengi na utandawazi umetamalaki” na misemo hii haijaishia tu kwa watu wa kidunia tu hapana! lakini imeenea na kuingia hadi makanisani kwa watu waliokoka (inashangaza sana).
Unamkuta mtu yupo katika wokovu, ni mtumishi mzuri tu, lakini unamsikia akisema maisha matakatifu kuishi ni ngumu sana, sasa kama wewe uliyempokea Yesu Kristo maishani mwako unasema haiwezekani, je! walio nje wasemeje? Mpendwa, tambua kwamba kuishi maisha matakatifu na yakumtii Mungu Inawezekana kabisa, hebu watafakari vijana hawa Danieli, Shadraki, Meshaki na Abednego ambao walipoletewa vyakula najinsi vilivyokatazwa na Mungu wao, walikataa na kuamua kujitunza nafsi kumpendeza Mungu tu. Hawakutazama vijana wenzao wanafanya nini, hawakutazama vijana wenzao wamechukua uamuzi gani, bali wao walikusudia kumtii Mungu tu.
Danieli 1:5 Huyo mfalme akawaagizia posho ya chakula cha mfalme, na ya divai aliyokunywa, akaagiza walishwe hivyo muda wa miaka mitatu; ili kwamba hatimaye wasimame mbele ya mfalme.
6 Basi katika hao walikuwapo baadhi ya wana wa Yuda, Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria.
7 Mkuu wa matowashi akawapa majina; alimwita Danieli, Belteshaza; na Hanania akamwita Shadraka; na Mishaeli akamwita Meshaki; na Azaria akamwita Abednego.
8 Lakini Danieli aliazimu moyoni mwake ya kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme, wala kwa divai aliyokunywa; basi akamwomba yule mkuu wa matowashi ampe ruhusa asijitie unajisi.
Hivyo na sisi tunatakiwa kuwa kama hao kumtii Mungu katika mazingira yoyote yale, Lakini endapo tukisema mazingira ya utandawazi ni kikwazo kisha na sisi tuendane nayo, na sisi tuwe watu wa kukaa vijiweni kusikiliza maneno yasiyofaa, au muda mwingi kutazama tamthilia, kutazama picha chafu mtandaoni nk hapo hatutoweza hata kidogo, lakini ukiamua kukaa uwepo mwa Mungu kwa kuhubiria wengine, kusoma neno la Mungu, kushiriki ibada za mkesha, kukutanika na watakatifu wenzako katika kumwabudu Mungu, kupitia kufanya hivyo kwa kuutoa mda wako kuutafuta uso wa Mungu kuishi maisha matakatifu itakuwa rahisi maishani mwako.
Bwana atusaidie, Shalom.