Elimu juu ya ndoto imetanuka kidogo, Ndoto zimegawanyika katika makundi makuu matatu,
1) Ndoto zinazotengenezwa na miili yetu wenyewe (Mhubiri 5:3):
Ndoto hizi zinakuja kutokana na shughuli mtu alizokuwa anazifanya kabla ya kulala au anazozifanya kila siku… Hiyo inasababisha ubongo wake kutawaliwa sehemu kubwa na shughuli hiyo, hivyo ni rahisi anapolala kuota yupo katika hiyo shughuli, au unakuta mtu anatazama filamu fulani, ni rahisi wakati wa kulala kuota kile alichokuwa anakitazama.
2) Ndoto zinazotengenezwa na shetani.
Hizi zinatengenezwa na yule mwovu na kutumwa ndani ya mtu, Hizi ni ndoto zote zenye maudhui ya kumfanya mtu aikane au aiache IMANI, au zinampelekea mtu aende mbali na mpango wa Mungu, au kutenda dhambi na huwa zinaambatana na ushawishi fulani mkubwa sana mara baada ya kuamka.
kwamfano mtu anaota kaachana na mume au mke wake na kupata mwingine ambaye ni mrembo au mzuri kuliko yule wa mwanzo, na asubuhi baada ya kuota ndoto hiyo, anaanza kuona kero ya kuishi na mke aliyenaye au mumewe kama mwanzo au hata anashawishika kumkimbia.
Au unakuta mtu anaota mama yake ni mchawi na hamtakii mema, na ndoto inamwambia au amchukieau ajitenge naye. Au mwingine anaota anafanya tendo la ndoa na mtu anayemfahamu, na anajikuta akiamka asubuhi ile roho ya tamaa bado inawaka ndani yake.
Au mtu anaota kapata utajiri kwa kumwibia mwajiri wake, au kwa kucheza kamari , na baada ya kuamka anajisikia msukumo ndani yake wa kwenda kufanya jambo lile na wakati mwingine mazingira aliyoyaona kwenye ndoto ndio hayo hayo anayaona akiwa nje ya ndoto kana kwamba ni unabii unatimia..
Au mwingine mtu anaota ndoto yupo kwa mganga wa kienyeji, akafanikiwa na anapoamka anashawishika kufanya mambo yale, au mtu anajikuta anaota kuna sanamu au kuna mti mkubwa mahali fulani umebeba mafanikio yake (pengine katika maeneo yake na kwenye ndoto anaona ameukata ule mti na mambo yote yakaharibika, na anapoamka anajikuta anatamani kuuheshimu ule mti zaidi.
Au wakati mtu anaota ametenda dhambi na Mungu hataki kumsamehe, na asubuhi anajikuta anawasiwasi Mungu hataki kumsamehe. Au ndoto nyingine mtu anaota amekufa baada ya kujaribu kumpa Yesu maisha yake.
Sasa ndoto kama hizi ni za yule Adui shetani kwasababu malengo yake ni kumlazimisha mtu asilitii Neno la Mungu bali alivunje, zinamtuma mtu kutenda dhambi zaidi kuliko kumfanya kuwa mtakatifu, au zinamfanya mtu awe na hofu zaidi kuliko kumpenda! N.k
Namna ya kuzidhibiti hizi ndoto ni kuamua kuishi maisha masafi yampendezayo Mungu na kujifunza kwa kina Neno la Mungu ili shetani anapoleta mawimbi yake kama bahari uwe na uwezo wa kuyadhibiti, Kadhalika na kudumu katika maombi. kwamfano mtu anayeoota kafanya kosa na hasamehewi, hiyo ni mishale ya shetani kutaka kukuvunja moyo usitake kuendelea kumtafuta Mungu, kwahiyo kama Neno halipo ndani yako linalosema
“1Yohana 1: 9 “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. ” hutaweza kumshinda shetani.
Au ndoto inapokuja umegombana na mke wako na umeachana naye na kupata mwingine bora kuliko huyo, utajua imetoka kwa yule mwovu kwasababu Neno la Mungu limekaa ndani yako linalosema
“Luka 16:18 Kila amwachaye mkewe na kumwoa mke mwingine azini; naye amwoaye yeye aliyeachwa na mumewe azini. ”
3)Aina ya tatu ya ndoto ni ndoto zinazoletwa na Mungu.
Lengo la ndoto hizi ni kumwonya mtu au kumuimarisha katika imani, Na aziji kwa wingi sana. Mfano wa ndoto hizi ni pale mtu anapoota anahubiriwa na kuonywa kuhusu maisha ya dhambi anayoishi. Na mfano mwingine wa hizi ndoto ni pale mtu anapoota Bwana Yesu karudi na kawanyakua watu wake, na anapoamka asubuhi anashawishika kujihakiki maisha yake ya wokovu yanaendaje.
Kwahiyo kwa ufupi ndoto zote zinazotoka kwa Mungu utazihakiki pia kama Neno la Mungu linalo kaa ndani yako, ndoto yoyote ile inayokupeleka kumtafuta Mungu zaidi na kutubu, au kukuonya tabia uliyonayo ambayo si ya KiMungu basi fahamu kuwa ndoto hiyo inatoka kiMungu.
Ayubu 33:14 “Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali.
15 Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani;
16 Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia muhuri mafundisho yao,
17 Ili amwondoe mtu katika makusudio yake, Na kumfichia mtu kiburi;
18 Yeye huizuia nafsi yake isiende shimoni, Na uhai wake usiangamie kwa upanga.
19 Yeye hutiwa adabu kwa maumivu kitandani mwake, Na kwa mashindano yaendeleayo daima mifupani mwake;