Nini maana ya kuota unajenga Nyumba, ngome, mji au mnara?
Ndoto hizi zimegawanyika katika sehemu kuu tatu , 1) Unaota unajenga nyumba lakini haiishi, au unaishia katikati 2) Unaota unajenga nyumba inakamilika lakini baadaye inaanguka au unanyang’anywa. 3) Unaota unajenga nyumba na inakamilika vizuri.
Tutaangalia kundi moja baada ya lingine.
- Unaota unajenga nyumba lakini haiishi.
Kama wewe umempokea Yesu, (yaani umeokoka vizuri) na kisha ukajikuta umeota ndoto ya namna hii, basi kuna uwezekano mkubwa sana, ikawa ni ujumbe wa Mungu kwako.
Nyumba au kitu chochote mtu anachoweza kukijenga siku zote vinawakilisha “Huduma ya Mtu” au “Wito wa Mtu”. Mtu aliyeitwa na Mungu na kuanza kumtumikia katika nafasi yoyote Mungu aliyomweka, katika roho ni sawa na anajenga nyumba au mnara au ngome. Hivyo kila mtu anajua jinsi anavyoijenga nyumba yake, wako walio hodari na walio dhaifu. Mtu dhaifu ni Yule ambaye hayupo makini na wokovu wake, katika roho anakuwa anaijenga nyumba yake kilegevu. Na inapotokea kaacha kabisa wokovu au karudi nyuma, basi katika roho nyumba yake hiyo inakuwa imesimama haiendelei kupanda, ndicho Bwana Yesu alichosema katika..
Luka 14:27 “Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
28 Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia?
29 Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki,
30 wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza”.
Kwahiyo ni lazima kuhakikisha unapiga gharama zote kabla ya kumfuata Bwana Yesu, vile vile unajikana nafsi katika kuishi maisha ya kikristo, ulegevu wa aina yoyote baada ya kumfuata Yesu, inatafsirika kiroho kama kazi iliyosimama
2) Unaota unajenga nyumba inakamilika lakini baadaye inaanguka au unanyang’anywa.
Nyumba kuanguka ni kuonyesha kuwa haikujengwa katika msingi ulio imara, maana yake ni kwamba, Mafundisho ya awali mtu aliyoyapokea kumhusu Yesu yalikuwa dhaifu, au mtu huyo hakumwelewa Bwana Yesu kama alivyopaswa kumwelewa, au aliyachukulia juu juu tu maneno ya Bwana Yesu, na akaendelea hivyo hivyo, katika kumtumikia Mungu..
Mathayo 7:26 “Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga;
27 mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa”.
3) Unaota unajenga nyumba na inakamilika vizuri.
Kuota unajenga nyumba na inakamilika na inadumu, ni ishara nzuri kuwa Huduma yako inaendelea vizuri au itaendelea vizuri katika roho, Lakini kwasababu ujumbe umekuja kwa njia ya ndoto, bado inakuwa ni tahadhari kwamba, huna budi kudumu katika imani, ili mambo hayo yatimie kama ulivyoyaona, shetani asiyaharibu, Kwasababu biblia inasema.
Ufunuo 3:11 “Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako”.
Ikiwa bado hujampokea Yesu na umeota ndoto hizo na kwa bahati umekutana na ujumbe huu, basi Bwana amekukusudia uokoke ili ushiriki Baraka zake. Mpokee Yesu na ukabatizwe.