Lipo jambo muhimu sana ambalo unapaswa kulitafakari wewe kama Mkristo (yaani wewe uliye mkiri Yesu Kristo kwa kinywa chako na kumwamini moyoni mwako) sawa sawa na andiko la
Warumi 10:10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.
Na kubatizwa katika ubatizo sahihi ambao ni wa kuzamishwa katika maji na kwa jina la Yesu Kristo sawasawa na
Matendo 2: 38 Petro akawaambia, Tubuni MKABATIZWE KILA MMOJA WENU KWA JINA LAKE YESU KRISTO, mpate ondoleo la dhambi zenu, NANYI MTAPOKEA KIPAWA CHA ROHO MTAKATIFU.
Sasa swali la kujiuliza wewe Mkristo ni je! maisha yako ya wokovu uliyo nayo sasa yana utofauti na yale uliyokuwa nayo zamani kabla ya kumpokea Kristo? Kwa sababu biblia inasema mtu akiwa ndani ya Kristo anakuwa kiumbe kipya.
2 Wakorintho 5:17 Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa KIUMBE KIPYA; YA KALE YAMEPITA TAZAMA! YAMEKUWA MAPYA.
Maana yake ni kwamba, kama bado hakuna utofauti wowote ule katika maisha yako basi haupo sawa katika wokovu wako, dada wa Kikristo, Jitafakari mwenyewe kama je! bado unavaa suluari kama zamani? Bado unavaa vimini kama zamani? Bado unavaa nguo zinazochora maungo yako na kuonesha sehemu za ndani za mwili wako kama mapaja, mgongo n.k? Bado unasuka nywele kichwani mwako? Bado unasuka mitindo ya kidunia kichwani mwako? Bado unaweka nywele bandia, kope bandia kucha bandia, make up, na lipstick kama zamani? bado unajichubua kama zamani, bado unavaa mahereni, mikufu, cheni na vikuku kama zamani?
Jitafakari dada wa kikristo, je! Bado unaendelea kufanya uasherati na boyfriend wako kama zamani? Bado unaendelea kuvumisha uongo na umbea kama zamani? Bado ni msengenyaji na mtukanaji kama zamani? Bado unaenda kwenye kumbi za anasa na starehe kama zamani?
Dada wa kikristo, kama bado unaendelea na vitu hivi na huku unasema wewe ni mkristo, basi tambua kuwa unajidanganya mwenyewe, hivyo fanya bidii kujirekebisha.
Kaka wa kikristo, Jitafakari mwenyewe kama je! Bado unaendelea na ulevi kama zamani, uvutaji sigara na kubeti kama zamani? Bado unaendelea kuvaa suruali zinazochora maungo yako kama zamani, bado unanyoa kimitindo na kuvaa milegezo kama zamani? Bado unaendelea kuvaa suruali zilizochanika chanika kama zamani, bado unaendelea kuvaa nguo za wanawake, bado unaendelea na kusuka nywele kama zamani? Bado unaendelea kusema uongo, kutukana matusi, kusikiliza miziki ya kidunia kama zamani?
Jitafakari kijana wa kikristo, je! bado unaendelea kufanya uasherati kama zamani? Bado unaendelea na Kupiga punyeto na kutazama picha za ngono kama zamani? Kama bado na huku unasema ni mkristo, tambua kuwa unajidanganya, kwa sababu bado hujauvua utu wako wa zamani na matendo yako kama biblia inavyosema.
Wakolosai 3:9 Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake;
Baba wa kikristo, Jitafakari mwenyewe kama je! Bado unaendelea kuishi na mwanamke ambaye si wako kama zamani? Na huku mke wako wa ndoa umemtelekeza (machukizo kwa Bwana), je! Bado unaishi na mke wa mtu kama zamani? Bado unakula rushwa na kutoa hongo kama zamani? Hebu Jitafakari Mkristo, kama bado unaendelea na vitu hivyo na huku unajiita mkristo basi tambua kuwa unajindanganya, maandiko yanasema uzae matunda yanayoendana na kutubu kwako.
Mathayo 3:8 Basi zaeni matunda yapasayo toba;
HII NI TAFAKARI KWAKO MKRISTO.
Shalom.