Katika kipindi hiki tulichopo cha siku hizi za mwisho, ni kipindi kibaya sana, ni kipindi cha kizazi kiovu na kibovu mno kinachojulikana kama KIZAZI CHENYE UKAIDI (Matendo 2:40), kizazi ambacho kinapingana na kushindana na kweli ya Mungu, kizazi ambacho hakitaki kulitii neno la Mungu, kizazi ambacho watumishi wa Mungu hawataki kusema kweli ya Mungu bali wanachochea dhambi, kizazi ambacho kinachukia utakatifu (si wakristo si watu wa mataifa), na kibaya zaidi kinasahau kwamba, pasipo utakatifu hakuna mtu atakayemwona Mungu.
Waebrania 12:14 Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, NA HUO UTAKATIFU, AMBAO HAPANA MTU ATAKAYEMWONA BWANA ASIPOKUWA NAO;
Tunasahau kwamba, hata kama tunaimba vizuri, hata kama ni wana maombi, hata kama ni manabii na waonaji wa maono makubwa makubwa, hata kama tunafundisha vizuri, pasipo utakatifu hakuna atakayeweza kumwona Mungu
Lakini kikazi hiki ni cha ajabu, hakitaki kuambiwa ukweli na tena kinachukia sana na kukasirika pindi kinapokemewa dhambi zao, kinapenda kubembelezwa bembelezwa katika dhambi zao na ukaidi wao (hiyo ndio furaha yao), yaani wanapenda kusikia injili laini kutoka kwa watumishi wa uongo wanapowaambia pokea gari, pokea nyumba, pokea mashamba, pokea mume au mke (injili zinazopendeza mioyo yao), na wakati huo huo wakisikia habari ya kutubu, kuacha dhambi na kuishi maisha matakatifu, sura zina badilika, mpendwa huna budi kuitii injili ya kweli kwani kwa hiyo hutaweza jiokoa nafsi yako na moto wa Jehanam, haijalishi itakukwaza kwa jinsi gani na kukuumiza kwa jinsi gani, injili ya kweli (neno), itakuweka huru rohoni utakapoamua kuitii kama Bwana alivyosema.
Yohana 8:32 tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.
Na tena ukiifahamu hiyo Kweli hakuna jambo lolote la kidunia kama fashion au mafundisho ya uongo yatakayo kutoa katika njia hiyo kwa sababu kweli unayo
ndani yako. Ukweli unauma ndiyo, lakini UNAPONYA, umeoka lakini bado ni mlevi, bado ni mzinzi, mwasherati, muongo, msengenyaji, mlawiti, unashiriki ndoa za jinsia moja, mvutaji wa sigara, na mchonganishi. Ndugu, acha mara moja ukaidi na uitii injili ya kweli inayosema.
1 Wakorintho 6:9 Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,
10 wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi.
Wewe ni mwanamke umeokoka lakini bado unavaa vimini na unavaa suluari, na kibaya zaidi kanisani. Unasema umeokoka dada lakini unapaka make up, unaweka makucha bandia, unasuka rasta, unaweka kope bandia, unabadili nywele rangi, unajiongezea shepu, unajichubua, unachora tatoo, unapaka hina, unapaka rangi kucha, uvaa hereni na vikuu, mpendwa acha ukaidi wako na uitii injili ya Kristo inayotuonya…. kwamba yote hayo ni Dhambi acha mapema wewe mwanamke na uishi katika uhalisia aliokupa Mungu.
1 Timotheo 2:9 Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;
10 bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu.
Acha kufuatisha jinsi duniani inavyoenda bali utoe mwili wako kuwa dhabihu takatifu na ya kumpendeza Mungu kama maandiko yanavyosema katika.
Warumi 12:1 Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.
2 Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.
Tii injili ya kweli, acha ukaidi na usifurahie dhambi.
Shalom